Genesis 35

Yakobo Arudi Betheli

1Kisha Mungu akamwambia Yakobo, “Panda uende Betheli ukakae huko na ukamjengee Mungu madhabahu huko, Yeye aliyekutokea ulipokuwa unamkimbia Esau ndugu yako.”

2Hivyo Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake pamoja na wote waliokuwa naye, “Iondoeni miungu ya kigeni ile iliyoko katikati yenu, jitakaseni na mkabadilishe nguo zenu. 3Kisha njooni, twende Betheli, mahali nitakapomjengea Mungu madhabahu, aliyenijibu katika siku ya shida yangu, ambaye amekuwa pamoja nami popote nilipokwenda.” 4Kwa hiyo wakampa Yakobo miungu yote ya kigeni waliyokuwa nayo, pamoja na pete zilizokuwa masikioni mwao. Yakobo akavizika chini ya mti wa mwaloni huko Shekemu. 5Kisha wakaondoka, na hofu ya Mungu ikawapata miji yote iliyowazunguka. Kwa hiyo hakuna aliyewafuatia wana wa Yakobo.

6Yakobo na watu wote waliokuwa pamoja naye wakafika Luzu (ndio Betheli), katika nchi ya Kanaani. 7Huko akajenga madhabahu na akapaita mahali pale El-Betheli,
El-Betheli maana yake Mungu wa Betheli.
kwa sababu mahali pale ndipo Mungu alipojifunua kwake alipokuwa akimkimbia ndugu yake.

8Wakati huu Debora, mlezi wa Rebeka, akafa na akazikwa chini ya mti wa mwaloni ulioko chini ya Betheli. Kwa hiyo pakaitwa Alon-Bakuthi.
Alon-Bakuthi maana yake Mwaloni wa Kilio.

9Baada ya Yakobo kurudi kutoka Padan-Aramu, Mungu alimtokea tena na kumbariki. 10Mungu akamwambia, “Jina lako ni Yakobo, lakini hutaitwa tena Yakobo, jina lako utakuwa Israeli.” Kwa hiyo akamwita Israeli.

11Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mwenyezi Mungu,
Mwenyezi Mungu hapa ni jina la Kiebrania, El-Shaddai (yaani Mungu Mwenye utoshelevu wote).
ukazae na kuongezeka. Taifa na jamii ya mataifa itatoka kwako, nao wafalme watatoka viunoni mwako.
12Nchi niliyowapa Ibrahimu na Isaka nakupa wewe pia, nami nitawapa wazao wako baada yako.” 13Kisha Mungu akapanda juu kutoka kwake mahali pale alipozungumza naye.

14Yakobo akasimamisha nguzo ya jiwe mahali pale Mungu alipozungumza naye, akamimina sadaka ya kinywaji juu yake, pia akamimina mafuta juu yake. 15Yakobo akapaita mahali pale Mungu alipozungumza naye Betheli.
Betheli maana yake Nyumba ya Mungu.

Vifo Vya Raheli Na Isaka

16Kisha wakaondoka Betheli. Walipokuwa umbali fulani kabla ya kufika Efrathi, Raheli akaanza kusikia uchungu na alipata shida kuu. 17Alipokuwa katika shida hii katika kujifungua, mkunga akamwambia, “Usiogope, kwa sababu umempata mwana mwingine.” 18Hapo alipopumua pumzi yake ya mwisho, kwa maana alikuwa akifa, akamwita mwanawe Benoni.
Benoni maana yake Mwana wa huzuni yangu.
Lakini babaye akamwita Benyamini.
Benyamini maana yake Mwana wa mkono wangu wa kuume.

19Kwa hiyo Raheli akafa, akazikwa kando ya njia iendayo Efrathi (ndio Bethlehemu). 20Juu ya kaburi lake, Yakobo akasimamisha nguzo, ambayo mpaka leo inatambulisha kaburi la Raheli.

21Israeli akaendelea tena na safari yake na kupiga hema mbele mnara wa Ederi. 22Wakati Israeli alipokuwa akiishi katika nchi ile, Reubeni mwanawe alikutana kimwili na suria wa baba yake aitwaye Bilha, naye Israeli akasikia jambo hili.

Yakobo alikuwa na wana kumi na wawili:

23 Wana wa Lea walikuwa:
Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Yakobo,
Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari na Zabuloni.

24 Wana wa Raheli walikuwa:
Yusufu na Benyamini.

25 Wana waliozaliwa na Bilha mtumishi wa kike wa Raheli walikuwa:
Dani na Naftali.

26 Wana waliozaliwa na Zilpa mtumishi wa kike wa Lea walikuwa:
Gadi na Asheri.

Hawa walikuwa wana wa Yakobo, waliozaliwa kwake akiwa Padan-Aramu.

27Yakobo akarudi nyumbani kwa baba yake Isaka huko Mamre, karibu na Kiriath-Arba (yaani Hebroni), ambapo walikuwa wameishi Ibrahimu na Isaka. 28Isaka aliishi miaka 180. 29Kisha Isaka akapumua pumzi yake ya mwisho akafa, akakusanywa pamoja na watu wake akiwa mzee wa miaka mingi. Nao wanawe Esau na Yakobo wakamzika.
Copyright information for SwhKC